Sunday, August 14, 2011

Bolton yavuna, Liverpool yavutwa shati

Sebastian Larsson alifunga bao maridadi sana la kusawazisha na kufanikiwa
kuipatia timu yake ya Sunderland pointi moja dhidi ya Liverpool katika
mechi ya ufunguzi wa Ligi Kuu ya Soka ya England.
Wenyeji Liverpool ilikuwa wapate bao mapema lakini mkwaju wa penalti
uliopigwa na Luis Suarez ukapaa juu la lango la Sunderland. Suarez
alisukumwa na mlinzi Kieran Richardson, lakini dakika chache baadae
akarekebisha makosa na kufunga bao la kwanza kwa Liverpool baada ya
kuunganisha kwa kichwa mkwaju uliochongwa na Charlie Adam.

Sunderland katika kipindi cha kwanza hawakuonekana tishio sana langoni mwa
Liverpool, lakini katika dakika ya 57 Larson alipata nafasi ya kuunganisha
mkwaju wa pembeni uliopigwa na Ahmed El Mohammedy na kuisawazishia timu
yake kwa bao safi sana huku ngome ya Liverpool ikiwa inamuangalia tu bila
kumkabili.

Matokeo hayo yamezifanya timu hizo zigawane pointi moja.

Nayo QPR imeanza Ligi Kuu ya soka ya England kwa kupachikwa mabao manne
huku Bolton ikiwafundisha soka katika mechi yao ya kwanza ya kufungua
msimu wa Ligi Kuu ya England.
Timu hiyo ya QPR ikicheza katika uwanja wa nyumbani ilicheza vizuri
kipindi cha kwanza, lakini wakawa wanazorota kila muda ulivyokuwa
ukiyoyoma.

Mabao hayo manne ya Bolton yalifungwa na Gary Cahill kwa mkwaju wa mbali
kipindi cha kwanza, Danny Gabbidon mlinzi wa QPR akajifunga mwenyewe bao
la pili na Ivan Klasnic akapachika bao la tatu.

Fabrice Muamba alikamilisha kitabu cha mabao kwa kufunga bao la nne, kabla
ya mchezaji wa QPR kutolewa nje kwa kadi nyekundu.

Matokeo hayo yanaifanya Bolton kuanza ligi kwa kuongoza ikiwa na pointi 3
na mabao manne.

Wolverhampton Wanderers ikiwa ugenini imeshalazwa bao 1-0, ilijipapatua na
kuweza kurejesha bao na hatimaye kufanikiwa kuilaza Blacburn mabao 2-1.
Blackburn Rovers walitangulia kufunga baada ya Jason Roberts kumtangulizia
mpira Mauro Formica ambaye mkwaju wake wa chini ulimshinda mlinda mlango
Wayne Hennessey.

Lakini Wolves ilijiuliza na kusawazisha bao lililofungwa na Steven
Fletcher kwa kichwa kutokana na krosi iliyochongwa na Matt Jarvis.

Stephen Ward aliipatia bao la ushindi Wolves kwa mkwaju wa juu baada ya
Kevin Doyle kukosa mkwaju wa penalti.

Nayo timu mpya iliyopanda ligi msimu huu ya Norwich ilipigana kiume na
kuweza kuilazimisha Wigan kutoka nayo sare ya kufungana bao 1-1, katika
mechi ya kufungua msimu huu.
Wigan walikuwa wa kwanza kufunga bao katika kipindi cha kwanza kupitia kwa
Ben Watson kwa mkwaju wa penalti baada ya Ritchie de Laet kuangushwa na
Franco di Santo.

Norwich walisawazisha wakati mpira ukielekea mapumziko kwa bao la Wes
Hoolahan kutokana na makosa ya mlinda mlango Ali Al-Habsi.

Mechi nyingine ilikuwa ni kati ya Fulham waliowakaribisha Aston Villa,
ambapo mechi hiyo haikushuhudia mabao, baada ya timu hizo kushindwa
kufungana hadi dakika tisini za mchezo.

No comments:

Post a Comment