Sunday, July 24, 2011

PAULSEN, Wachezaji kuweni kama Ngasa na Nizar

KOCHA wa timu ya Taifa, 'Taifa Stars' Jan Poulsen amewataka wachezaji wanaounda kikosi cha timu ya Taifa ya Vijana U-23 kufuata nyayo za Mrisho Ngassa na Nizar Khalfan waliocheza dhidi ya Manchester United na Manchester City ili hapo baadaye Tanzania iweze kupata wachezaji walio katika viwango bora na kufanya vema katika mashindano mbalimbali.

Poulsen aliwaambia wachezaji hao jana jijini Dar es Salaam wakati akijaribu kufuatilia viwango vya wachezaji watatu Gaudence Mwaikimba (Moro Utd), Haruna Moshi (Simba) na Juma Seif (Yanga) aliowataka kujiunga na kikosi hicho kwa lengo la kufuatilia uwezo wao na kuwajumuisha kwenye kikosi cha Taifa Stars kitakachoanza maandalizi ya kujiandaa na mchezo dhidi ya Algeria.

Kikosi cha timu ya Taifa ya vijana U-23 chenyewe kinajiandaa na mechi mbili za kirafiki za kimataifa dhidi ya Shelisheli zitakazochezwa kwenye uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha Julai 27 na 30.

"Nimepata faraja kubwa sana kumuona Mrisho Ngassa akicheza dhidi ya Manchester United, ambapo timu yake ya Seattle Sounders ya Marekani ilifungwa mabao 7-0,"

"Alicheza vizuri tofauti na nilivyofikiri, ni jambo la kujivunia kwa Tanzania na Ngassa (Mrisho) mwenyewe, hakuna jambo zuri linakuja bila ya kujituma mwenyewe na kujiwekea malengo na nidhamu," alisisitiza Poulsen.

"Nilivutiwa pia na Nizar Khalfan alivyocheza dhidi ya mabingwa wa kombe la FA nchini Uingereza, Manchester City, alionyesha kujiamini na mpira wakati wote wa mchezo ule," alisema.

Alisema wachezaji Nizar Khalfan wa Voncouver Whitecaps ya Canada alicheza dhidi ya Manchester City ambapo timu hiyo ilichapwa kwa mabao 2-1 na Mrisho Ngassa wa Seattle Sounders dhidi ya Manchester United na kuonyesha kwamba Tanzania inaweza isipokuwa ni wachezaji wenyewe hawataki kujaribu bahati hizo na kuweka malengo ya kufika mbali.

"Wachezaji wengi wa Tanzania wameridhika na soka la hapa nyumbani kitu ambacho sio sahihi kwao endapo wanahitaji nchi yao iweze kusonga mbele lazima kuongeza juhudi na kujaribu kucheza soka la kulipwa kwa ajili ya kujifunza mengi zaidi kutokana na changamoto," alisema Poulsen. 

No comments:

Post a Comment