Friday, July 15, 2011

Pazia la uhamisho kufungwa leo

SHIRIKISHO la soka nchini TFF,  limetangaza leo kuwa mwisho wa uhamisho wa wachezaji kwa klabu zote za Ligi Kuu na zimewakumbusha kuhakikisha mpaka ifikapo Julai 20 kukamilisha zoezi zima la usajili wa wachezaji wao kwa msimu ujao wa ligi.

Aidha TFF wamezitaka klabu za Simba na Yanga kuhakikisha zinakamilisha taratibu zote endapo watahitaji kutumia uwanja wa Taifa katika ligi kuu ikiwemo kuridhia gharama za uwanja huo.

Afisa habari wa Shirikisho hilo, Boniface Wambura alisema jijini jana kuwa walitoa muda wa kutosha kwa klabu zote kufanya zoezi la uhamisho pamoja na usajili wa wachezaji hivyo kwa sasa hawatahusika na malalamiko yoyote kuhusiana na uhamisho wa mchezaji yeyote.

Alifafanua kuwa suala la uhamisho hawatahusika nalo mara baada ya tarehe kupita, lakini amedai klabu zitaendelea kusajili wachezaji hadi Julai 20 ambapo ndipo itakuwa mwisho kabisa.

"Napenda kuzikumbusha klabu kuwa kesho (leo) itakuwa mwisho wa uhamisho wa wachezaji kutoka klabu moja kwenda nyingine ila usajili utaendelea kama kawaida hadi hapo tarehe iliyopangwa ifike...cha msingi wakae na kuweka mambo yao vizuri na kuanzia sasa sisi tupo tayari kupokea majina kwa klabu yoyote itakayokuwa imekamilisha zoezi lake,"alisema Wambura.

Aidha Wambura alisema wamepokea barua za maombi ya klabu za Simba na Yanga zinazouomba kutumia uwanja wa Taifa katika ligi kuu na Tff inazitaka klabu hizo  kuhakikisha zinakamilisha sheria zote zinazohitajika ili ziweze kuruhusiwa kuutumia uwanja huo.

Kwa upande wa Simba kupitia kwa Ofisa habari wao, Ezekiel Kamwaga alisema endapo TFF watawakubalia watakutana na Wizara ili kuweza kuomba kupunguziwa gharama za uwanja kutokana na kuwa kubwa kwao.

 

No comments:

Post a Comment