Wednesday, July 20, 2011

Vijana Stars waanza kambi

TIMU ya soka ya taifa ya vijana chini ya miaka 23, ‘Vijana Stars’ leo inaingia kambini kujiwinda na mchezo wa kirafiki wa kimataifa dhidi ya Seshar ya Shelisheli.
Mchezo huo unatarajiwa kufanyika Julai 27 kwenye uwanja wa Sheikh Amri Abeid mjini Arusha.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Kocha Mkuu wa timu hiyo, Jamhuri Kihwelu, alisema timu yake itaanza kwa mazoezi mepesi ambayo yatafanyika katika uwanja wa Karume.
Kihwelu alisema amewaita wachezaji 20 kuunda timu hiyo na kwamba wote wataanza mazoezi hayo mepesi kabla ya safari ya Arusha.
“Mchezo huo utasaidia kuimarisha timu yangu inayojiwinda na michuano ya Chalenji ya vijana,” alisema.
Michuano hiyo ya Chalenji imepangwa kufanyika Nairobi mwezi ujao. Wachezaji wanaounda timu hiyo ni Juma Abdul (Mtibwa Sugar), Himid Mao (Azam), Babu Ally (Morani), Shabani Kado (Yanga), Salum Abubakar (Azam), Godfrey Wambura (Simba), Jabir Aziz (Azam), Seif Juma (Ilala), na Khamis Mcha (Azam).
Wengine ni Shomari Kapombe (Simba), Jackson Wandwi (Azam), Issa Rashid (Mtibwa Sugar), Thomas Ulimwengu (Humbarg SV, Ujerumani), Hussein Javu (Mtibwa Sugar), Mohamed Soud (Toto Africans), Jamal Mnyate (Azam), Awadh Juma (Moro United), Salum Kanoni (Simba), Salum Telela (Yanga), Samuel Ngasa (African Lyon) na George Mtemahanji (Modeva FC, Italia).

No comments:

Post a Comment