Monday, August 29, 2011

VIINGILIO STARS NA ALGERIA VYATAJWA

Viingilio kwa ajili ya mechi ya mchujo kutafuta tiketi ya kucheza fainali
za Kombe la Mataifa ya Afrika zitakazofanyika mwakani nchini Equatorial
Guinea na Gabon kati ya Taifa Stars na Algeria vitakuwa kama ifuatavyo;
Akizungumza na waandishi wa habari msemaji wa Shirikisho la Mpira wa Miguu
Tanzania TFF Bw. Boniface Wambura amesema "Viti vya kijani ni sh. 3,000,
viti vya bluu sh. 5,000, viti vya rangi ya chungwa sh. 7,000, VIP C
sh.10,000, VIP B sh. 20,000 na VIP A sh. 30,000. Tiketi zitaanza kuuzwa
Septemba Mosi mwaka huu".
Taifa Stars tayari iko kambini tangu jana (Agosti 28 mwaka huu) na
inaendelea na mazoezi Uwanja wa Karume ambapo wachezaji wote wa ndani
waliripoti jana mchana na kuanza mazoezi jioni.
Wachezaji wan je waliofika jana usiku ni Abdi Kassim na Dan Mrwanda kutoka
Vietnam na Mbwana Samata kutoka Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo. Athuman
Machupa (Sweden), Henry Joseph (Norway) na Idrisa Rajab (Kenya) wanaingia
leo jioni.
Nizar Khalfan wa Vancouver Whitecaps ya Canada ndiye atakayekuwa mchezaji
wa mwisho kuripoti kambini. Khalfan atatua nchini kesho saa 5.15 usiku kwa
ndege ya PrescisionAir akitokea Nairobi.

No comments:

Post a Comment